Binti wa miaka 16 jijini Arusha alivyotumia Dola za Kimarekani 60,000 kuwanunulia marafiki zake taulo za kike

mtoto Arjun Kaur Mittal (katikati) akiwa na marafiki zake wa shule ya Mkonoo Mkoani Arusha.



Arusha.



Zaidi ya wanafunzi 400 katika shule ya sekondari Mkonoo Mkoani Arusha wamefanikiwa kugaiwa taulo za kike kwa ajili ya kuwasaidia kujisitiri wanapokuwa katika kipindi chao cha hedhi.

 


Wanafunzi hao wamepatiwa Taulo hizo za kike leo Agost 9,2024  na mtoto Arjun Kaur Mittal (16) kupitia kampeni yake ya ‘Her needs Tanzania’ yenye lengo la kuwafikia zaidi ya wanafunzi 10,000.



Wakipokea taulo hizo, mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo ya Mkonoo, Lucia Maiko mbali na kumshukuru Mittal kwa msaada huo lakini pia ameomba watu wengine kujitokeza kuwasitiri zaidi.


“Tunasema asante sana kwa mwenzetu kuona umuhimu wa kutusitiri, Kiukweli ni msaada mkubwa sana  kwani mabadiliko hayo ya kimwili yanayotukumba imekuwa ikitusababisha kushindwa kuhudhuria masomo kwa sababu ya kutojiamini hivyo tunaomba mashirika mengine yajitokeze kutusaidia taulo nyingi zaidi” amesema Lucia.


Nae Clara Kanuti ametumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuweka mpango wa kuwasambazia taulo hizo mashuleni ili kupunguza utoro katika kipindi cha hedhi hasa kwa wasichana wa jamii zenye hali duni kwani imekuwa ikishusha hadi taaluma yao.


Nae Binti Mittal aliyetoa msaada huo amesema kuwa alifikia uamuzi wa kuchangisha fedha kwa marafiki na ndugu zake wanaoishi nchini Dubai na India lakini pia Arusha Nchini Tanzania baada ya kugundua changamoto kubwa wanayokumbana nayo wanawake katika kipindi cha Hedhi.


“Naona changamoto ninazopitia nikiwa katika siku hizo za hedhi, lakini mimi nina uwezo wa kununua taulo hizi, hivyo nikapata picha ya wale walio katika familia duni wasioweza kununua nikajua uhitaji ni mkubwa nikaamua kuomba msaada kwa marafiki, ndugu na jamaa na nashukuru Mungu wameniunga mkono” amesema Mittal.



Amesema kuwa kwa sasa amefanikiwa kuchangisha dola za kimarekani 60,000 ambazo anatarajia kusaidia zaidi ya wasichana 10,000 kwa awamu ya awali ambapo atawasaidia kupata elimu ya hedhi salama, matumizi ya vifaa hivyo kwa usalama wao kiafya kipindi cha hedhi lakini pia kuwanunulia taulo za kike za kujisitiri.


Nae Mwalimu wa shule ya Mkonoo, Bernadetha Cosmas amesema kuwa changamoto za hedhi zimeshusha baaadhi ya wanafunzi kiwango cha taaluma yao kutokana na utoro au kuomba ruhusa na kukaa nyumbani kuanzia siku tano hadi 10 kila mwezi.


“Kikubwa serikali inavyoona umuhimu wa kuleta vitabu shuleni kwa ajili ya ufaulu, ione pia umuhimu wa kuleta na taulo hizi ili kustiri wanafunzi wanapokumbwa na hali ya hedhi kwani wengi wa jamii za pembezoni wanatoka familia duni ambao hawawezi kumudu kununua huku vipande vya vitambaa wanavyovaa zikiwasababishia magonjwa mbalimbali ikiwemo kuwashwa” amesema mwalimu Cosmas.



Kwa upande wake M’bunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo alimpongeza Mittal kwa kutoa msaada huo na kuwataka wadau wengine na mashirikia kujitokeza kusaidia wasichana kujistiri kipindi chao cha Hedhi.


“Elimu ni muhimu kwa watoto wetu hasa wasichana ambao wanakuja kuhudumia jamii kubwa baadae, hivyo niombe wadau wengine wajitokeze kuunga mkono jitihada hizi ili kufanikisha wanafunzi wengi zaidi kufikiwa na msaada huu” amesema Gambo.


Mwisho………

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post