![]() |
Watoto hao Mordekai Maiko(7) na Masiai Maiko(9) |
Hatimae imekuwa faraja ya hali ya juu moyoni mwa mwanamke Elizabeth Modesta (31) baada ya kusikia sauti ya watoto wake wawili wakiwa wazima wa afya tele baada ya kupita siku tatu akihaha kuwatafuta akijua wametekwa.
Watoto hao Mordekai Maiko(7) anaesoma darasa la tatu na Masiai Maiko(9)anaesoma darasa la Tano wote katika shule ya Msingi Olosiva iliyoko Wilayani Arumeru Mkoani Arusha, walitangazwa kupotea na mama yao baada ya kupandishwa daladala asubuhi julai 24,2024 kwenda shule lakini hadi jioni hawakurejea.
Baada ya kutoweka huko bila tarifa zozote, mama wa watoto hao alianza kuwatafuta shuleni na kwa marafiki bila mafanikio na badae kuamua kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi kuomba msaada ndipo upelelezi ukafanyika na kugundulika kuwa walichukuliwa na baba yao.
![]() |
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo |
Akithibitisha kupatikana kwa watoto hao, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo amesema kuwa watoto hao walichukuliwa na baba yao mzazi, Maiko Eliidi na kuwasafirisha hadi mji wa Migori ulioko nchini Kenya anakoishi.
“Baada ya kupokea taarifa hizi tulianza kuzifanyia kazi na kufanikiwa kujulikana watoto walikuwa na baba yao na taratibu sasa zinafanyika za kuwarudisha nchini baada ya kuwasiliana na mama yao mzazi kumtoa hofu ” amesema Masejo.
Kamanda amesema kuwa bado jeshi la Polisi halijajua sababu ya baba mzazi kutekeleza tukio hilo, hivyo upelelezi utaendelea ikiwemo kumhoji atakapofika nchini kwa ajili ya kuwarudisha watoto kama alivyoamriwa.
![]() |
Mama wa watoto hao, Elizabeth Modesta |
Akizungumzia tukio hilo, Mama mzazi wa watoto hao, Elizabeth amesema kuwa ni kweli amefanikiwa kuwasiliana na mzazi mwenzake na watoto pia wakiwa salama.
“Kwa wanavyoongea wanaonekana wako salama na furaha na nashukuru sana mtandao huu 'Habari Kaskazini ' kwa kuanza kusambaza taarifa hizi hadi nimefanikiwa kuwapata wanangu leo” amesema Elizabeth.
Amesema kuwa hadi sasa hajajua lengo la mzazi mwenzake kuwachukua watoto kinyemela bila kumtaarifu hivyo anasubiri watakapopata nafasi ya kukutanishwa ataweza kulizungumzia hilo.
“Imenipa mshtuko mkubwa sana hilo jambo, na imenipa mawazo makubwa kuwakosa watoto wangu, hivyo hata nilipothibitisha kuwa wako na baba yao bado sijaweza kuuliza sababu ya kufanya hivyo labda siku akitua nchini anaweza kuelezea” amesema Elizabeth.
Katika Ukurasa wake wa Instagram, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wanawake na Makundi maalum Dk Dorothy Gwajima ameposti picha ya watoto hao na kusema wamepatikana huku akionyesha wazi kufurahishwa na jambo hilo na watoto kupatikana.