![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda |
Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda amewaomba Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti ya Nelson Mandela kinachohusika na maswala ya Sayansi na Teknolojia Afrika, kufanya utafiti wa upatikanaji wa Teknlolojia ya uchujaji wa maji dhidi ya madini ya Flouride ambayo yamekuwa na madhara makubwa kwa wananchi wake.
Amesema kuwa miongoni mwa madhara wanayopata wananchi kwa sasa kutokana na matumizi ya maji yenye wingi wa Flouride ni pamoja na kupinda viungo hasa miguu, mikono na migongo lakini pia watoto wachanga kuzaliwa na vichwa vikubwa sambamba na kudhoofisha meno.
Kaganda ameyasema hayo kwenye Mkutano wa wanafunzi wa Utafiti wa mifumo ya maswala ya maji taka na kilimo uliofanyika kwenye Chuo cha Nelson Mandela kilichoko Arumeru Mkoani Arusha na kushirikisha Watafiti kutoka nchini Tanzania na Ubelgiji.
Akizungumza kwenye Mkutano huo, Kaganda amesema kuwa Wananchi wa wilaya yake hasa Kata ya Oldonyosambu na Oldonyowasi ni waathirika wakubwa wa maji wanayotumia kutokana na kuwa na wingi wa madini ya Flouride hivyo kuwaomba watafiti hao kutoka Tanzania na nchini Ubelgiji kuwekeza upya nguvu zao kwenye utafiti huo kuokoa kizazi cha wananchi wa sasa na baadae.
“Wingi wa madini haya unadhoofisha hadi mifupa na kuleta ulemavu kwa wananchi wangu na nadhani hata inapunguza umri wa kuishi wa wananchi wale kutokana na madhara hayo ya wingi wa madini hayo ambayo ni zaidi ya miligrame 2.5 tofauti na miligrame 1.5 inayotakiwa” amesema Kaganda .
Amesema kuwa katika suluhu ya tatizo hilo, Tafiti nyingi zimekwisha fanyika lakini zina uwezo wa kuchuja maji kiwango kidogo kwa ngazi ya familia tena wenye uwezo lakini tatizo bado kubwa kwenye maeneo ya umma hasa shule, hospitali na hata sehemu za halaiki kama masokoni.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Nelson Mandela, Professa Anthony Mshandete anaeshughulikia taaluma, utafiti na ubunifu, amesema kuwa wamekubali ombi la Mkuu wa Wilaya na watakaa kama wanataaluma kwa ajili ya kujadili swala hilo.
“Leo amekuja kufunga mkataba wetu wa ushirikiano kati ya Chuo cha Sayansi na Teknolojia Afrika cha Nelson Mandela na Wataalamu wa Utafiti kutoka vyuo vikuu vya Nchini Ubelgiji, ambao tulikuwa tunafanya mashirikiano ya utafiti wa mifumo ya maji taka kwa ajili ya kurudisha kwenye matumizi hasa ya kilimo cha Umwagiliaji wa ndizi”amesema Profesa na kuongeza;
“ Hivyo kwa sababu Mkuu wetu ameibua swala jipya, tutakaa kuona namna ya kufanikisha utafiti huo na tukikubaliana basi tutatembelea maeneo yenye madhara na kukusanya sampuli mbalimbali” amesema Professa Mshandete.
Akizungumzia mafanikio ya mradi huo, Profesa Mshandete amesema kuwa Wataalamu wa Utafiti nchini wamefanikiwa kuvuna Ujuzi, ubunifu na Teknolojia mbali mbali za kutibu maji taka na kurudisha kwenye matumizi tena hasa ya kilimo cha umwagiliaji.