Serikali waipiga pini Chaneta, wapewa kibarua cha kutatua migogoro yao,

 

Naibu Waziri mwenye dhamana ya michezo, Hamis Mohamed Mwinyijuma 


Arusha.

Serikali imewapa kibarua Chama cha Mchezo wa Netiboli nchini (Chaneta) kutatua migogoro yao ya ndani sambamba na kufanya uchaguzi mzuri wa wachezaji wa timu ya Taifa kwa kufuata haki.

Imesema kuwa kwa kufanya hivyo, Chaneta itapata nafasi ya kuruhusiwa kushiriki michuano mbali mbali ya kimataifa na kufadhiliwa na serikali lakini pia itawapatia wadhamini wa kudumu wa kusapoti mchezo huo.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri mwenye dhamana ya michezo, Hamis Mohamed Mwinyijuma wakati akifungua mkutano Mkuu wa Chaneta leo jumanne Julai 30,2024 jijini Arusha na kuhudhuriwa na wajumbe 76 kutoka mikoa yote 26 za Tanzania bara.



Katika mkutano huo, Mwinyijuma amesema kuwa Mchezo wa Netiboli ni moja ya michezo mitano iliyopewa kipaumbele na serikali na inafaa kuwa mchezo namba mbili unaofanya vizuri nchini lakini kutokana na migogoro inayoendelea baina yao na kupakana matope imesababisha mchezo huo kupoteza mvuto kabisa.

“Mchezo huu umeingizwa matopeni kwelikweli na umepoteza mvuto na umaarufu wake na hii imesababisha hata kukosa wadhamini maana hakuna mtu au taasisi anataka kuwekeza fedha zake kwenye vurugu hivyo basi nataka moja ya ajenda zenu hapa ninyi viongozi wa juu kuhakikisha mnayafanyia kazi hili na mnamaliza migogoro” amesema Mwinjuma;

“Lakini pia swala lingine linalowaponza ni namna dhaifu ya kuchagua timu yetu ya Taifa ya netiboli na maandalizi hafifu ambayo timu hiyo inapata, hivyo kuanzia sasa hivi tukishindwa kujiridhisha kama timu imechaguliwa kwa haki na kwa jinsi inavyofaa au imefanya maandalizi ya kutosha hatuwezi kuwaruhusu kwenda popote” amesema Mwinjuma.



Akitoa salamu za Shukrani Makamu Mwenyekiti wa Chaneta, Shyrose Bhanji amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Naibu waziri na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha mchezo huo unatimiza malengo yake ya kuwakilisha nchi vema kwenye michuano ya kimataifa.

“Ni kweli yote uliyayasema na tunaahidi baada ya mkutano huu, utapata mrejesho mzuri na tunakwenda kuanza moja dhidi ya mambo yote na zaidi tunakuahidi tutakwenda kukuletea timu bora na yenye ushindani msimu huu” amesema Bhanji.

Amesema malengo ya Mkutano huo ni kupitia katiba ili kuiboresha iendane na mahitaji ya netiboli kwa sasa na pia watapitia taarifa za fedha na mpango kakati wa netiboli.

Meneja wa Kanda ya Kaskazini kutoka Benki ya NMB, Baraka Ladislaus


Mmoja wa wadhamini wa Mkutano huo, Meneja wa Kanda ya Kaskazini kutoka Benki ya NMB, Baraka Ladislaus amesema kuwa wamesapoti mkutano huo kiasi cha Shilingi milioni nane ili kuwasaidia kufanikisha malengo waliojiwekea yatimie.

“Tumefanya hivi kwa kutambua umuhimu wa michezo kwenye jamii lakini pia kundi kubwa la wanamichezo ambao ni wateja wetu hivyo tutaendelea kuunga mkono jitihada za michezo nchini kumsaidia Rais wetu kuhakikisha wanafanikiwa kwenda kimataifa na kuitangaza nchi yetu vema” amesema Baraka.

Benki na NMB wakikabidhi mfano wa Hundi yao ya Shilingi milioni nane kusapoti Mkutano huo


Amesema, kufanya hivyo ni kuzidi kuisogeza Taasisi hiyo karibu na wananchi kujua changamoto zao lakini pia kubuni bidhaa mbalimbali zenye kuleta masuluhisho ya kifedha.

“Kwa sasa tunaendelea kutoa elimu jumuishi ya kifedha na kufungulia wateja  akaunti mpya ya NMB pesa kwa shilingi 1000 na inawasaidia kupata hadi mikopo ya mshiko fasta bila kudai makabrasha yoyote” amesema.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post