NMB wawatoa wanafunzi 160 makwao

Wa pili kushotoni Meneja wa Kanda ya kaskazini NMB, Baraka Ladislaus akitoa maelezo juu ya msaada wa vitanda 80 walivyovitoa katika shule ya msingi Same na Kimala sekondari vyenye thamani ya milioni 25.6, wanaefuata ni katibu tawala Wilaya ya Same Upendo Wela, na mwenyekiti wa halmashauri ya Same Yusto Mapande na kaimu mkurugenzi wa Same Cainan Kiswaga  wakiwa tiyari kwa ajili ya kuvipokea,



Bethy Mollel, Same


Jumla ya vitanda 80 vilivyotolewa na Benki ya NMB, kwa shule ya msingi ya wenye mahitaji maalum ya Same na Kimala Sekondari, imewezesha wanafunzi 160 kuhamia bweni na kuepukana na kutembea umbali mrefu kutoka makwao.


Msaada huo uliotolewa na Benki ya NMB umekabidhiwa na meneja wao Kanda ya kaskazini Baraka Ladislaus, kwa viongozi wa serikali ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro.


Akikabidhi vitanda hivyo meneja wa Benki ya NMB Kanda ya kaskazini, Baraka Ladislaus alisema kuwa vitanda hivyo vya juu na chini (double decker)  ni majibu ya maombi waliyoletewa na shule ya msingi Same inayolea watoto wenye mahitaji maalumu lakini pia shule ya sekondari Kimara.


"Kutokana na Elim ni moja ya kipaumbele cha Benki yetu ya NMB, ndio maana tumejibu haraka maombi yenu ya vitanda na leo tumeleta  80 vya kusaidia wanafunzi 160 kulala kutoka shule ya Same na vingine 40 vikienda shule ya Kimara vyote vikiwa na thamani shilingi milioni 25.6 ikiwa ni muendelezo wa kurudisha faida yetu katika kuhudumia jamii"

Alisema kuwa Benki ya NMB mwaka huu wametenga kiasi cha billion 6.2 kwa ajili ya kuhudumia jamii katika sekta ya mazingira, Afya, Elim na Majanga mbali mbali hivyo kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuisaidia serikali kutatua changamoto mbali mbali.

"Tunatambua juhudi kubwa za serikali chini ya Rais wetu Samia Suluhu za kusimamia upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, na sisi kama wadau tunao wajibu wa kuunga mkono, kusaidia na kuwa mstari wa mbele katika kuchagia utatuzi wa  changamoto zinazojitokeza katika jamii hivyo hatutachoka kuendelea kutoa misaada hii mara kwa mara itakapohitajika, alisema Baraka

Alisema kuwa wanaona umuhimu wa kurudisha kwa jamii kutokana na wao ndio msaada mkubwa walioifanikisha Benki hiyo kupiga hatua kubwa waliyonayo sasa.


Alisema kuwa moja ya mafanikio makubwa waliyoyapata ni kufungua matawi 229 na kusambaza mashine za kutokea huduma zaidi ya 800  huku wakiwa na zaidi ya mawakala 20, 000 nchi nzima


"Kwa sasa NMB tumefika mikoa na Wilaya zote nchini huku tukizindua kampeni mbali mbali za kutoa masuluhisho ya huduma za kifedha na mikopo kwa wateja wetu ikiwemo ',onja unogewe ' , lakini  'hati fungani' zinazomsaidia mteja kuwekeza fedha zake na kupata faida"


Akipokea msaada huo, kwa niaba ya serikali katibu tawala Wilaya ya Same Upendo Whela aliwashukuru NMB kwa vitanda hivyo akiwataka kuendelea kuisaidia serikali katika sekta ya vipaumbele vyao.


"Palipo na ukweli basi usemwe, na hii ni kwa Benki ya NMB walivyojipambanua katika kusaidia serikali kukwamua changamoto mbali mbali zinazoikabili wananchi, hakika mmekuwa mfano mkubwa na naomba msiache.


Mbali na shukrani hizo, Upendo aliwaomba NMB utayari wa kuisaidia serikali vifaa vya kujiandaa na uokozi sambamba na utiyari wa kuwasaidia wananchi watakaopataadhara dhidi ya mvua za El-nino zilizotabiriwa kuwepo katika msimu huu wa mvua za vuli kuanzia mwezi Octoba hadi desemba 2023.


"Hatuombei mvua hizi zitokee na hata zikitokea hatumtaki zilete madhara lakini maadam zimetabiriwa basi lazima tuchukue tahadhari mapema kupunguza madhara, hivyo tutakuja tena kuomba msaada tafadhali msituchoke" alisema Upendo

Mwenyekiti wa Baraza la halmashauri ya Same, Yusto Mapande akimkabidhi mwalim mkuu wa shule ya msingi wenye mahitaji maalumu Same Niwaeli Uwajia(kulia) sehemu ya vitanda 80 vilivyotolewa na Benki ya NMB vyenye thamani ya shilingi million 25.6, wengine kulia ni katibu tawala Wilaya ya Same Upendo Whela, akifuatiwa na meneja wa Kanda ya kaskazini NMB Baraka Ladislaus, meneja tawi la Same Emily Mkenda na meneja mahusiano Kanda ya kaskazini, Christabel Hizza.


Akikabidhiwa msaada huo, mkuu wa shule ya msingi Same, Niwaeli Uajia alisema kuwa vitanda hivyo vitatumika na wanafunzi wenye mahitaji maalum katika bweni walilojengewa na serikali hivi karibuni kwa fedha za Uviko-19 kiasi cha shilingi milioni 80.


"Tulijengewa bweni hili kutokana na mahitaji makubwa yaliyoonekana ya wanafunzi hawa hasa wenye mahitaji maalum kutokea mbali hali ambayo ni hatari kwa maisha yao, lakini hakukuwa na vitanda hali iliyoshindikana kupatumia, hivyo tunaishukuru Benki ya NMB kwa msaada huu ambao utaongeza tija kubwa ya masomo shuleni kwetu hasa uwezo wa kuwalaza wanafunzi wanaotoka mbali"




1 Comments

Post a Comment
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!