Bertha Mollel - Arusha.
. Kutokana na vifo
vingi vya vifaranga vinavyowatokea kwenye mabanda na vyakula kushindwa kukuza
kuku kwa mda unaotakiwa wafugaji nchini wameiomba serikali kudhibiti makampuni
yanayotoa vifaranga na vyakula vya kuku wa nyama visivyo na ubora kwani
vinawadidimiza kiuchumi.
Hayo yamesemwa na
wafugaji wa kuku wa nyama (Broiler) kwenye mkutano wa siku moja uliowakutanisha
wafanya biashara wa kuku na wafugaji kutoka mikoa ya Arusha, Manyara,
Kilimanjaro, Tanga na Dodoma iliyoitishwa na Kampuni ya bidhaa asilia za kuku
cha 'Trouw nutrition'
Mmoja wa wafugaji
Beatrice Mlay kutoka Moshi anaefuga kuku 500 alisema kuwa ufugaji wa kuku
umekuwa na changamoto nyingi zinazokatisha tamaa ya kuendesha shughuli hiyo
huku baadhi ya makampuni wakitoa bidhaa zisizo na ubora hali inayowadidimiza
kiuchumi.
"Miaka ya nyuma
ufugaji ulikuwa unalipa sana kiasi cha kuwa shughuli ya kipaumbele kwa vijana
wasio na ajira au wazee wanaostaafu lakini kwa sasa imekuwa inatunyonya hata
mitaji yetu kutokana na baadhi ya makampuni kutokuwa waaminifu na bidhaa
wanazotuuzia kwa kupunja baadhi ya virutubisho kwenye vyakula ili kujipatia faida"
alisema na kuongeza...
"Tunaomba
serikali ifanye msako wa viwanda vya vyakula bubu na wale wanazotengeneza
vyakula vizivyo na ubora wafungiwe, pia
mashamba ya kuzalisha vifaranga wakaguliwe maana siku hizi vifaranga vingi feki
havina ubora vinakufa vikifika bandani na wengine kudumaa bila kukua kwa muda
tarajiwa"
Alisema katika banda
lake analoingiza kuku 500 kuanzia siku ya kwanza hadi siku 35 anayopaswa kuuza,
hupoteza zaidi ya kuku 50 hadi 100 inayotokana na vifaranga dhaifu, lakini pia
ubora wa vyakula mdogo tena vingine vikiwa na sumu kuvu ambayo huharibu mfumo
mzima wa kupitisha chakula kwa kuku.
Nae Charles Shauri
anaefuga kuku 1000 alisema kuwa changamoto inayowakabili ni bei ndogo ya kuku
ya shilingi 6500 kwa mmoja huku kukiwa na bei kubwa ya vyakula vya kuku wa
nyama iliyokuwa inauzwa shilingi 60,000 hadi 65,000 kwa kiroba cha kilo 50
mwaka 2020 sasa ni 85,000 hadi 90,000 hali ambayo imepandisha pia bei ya
vifaranga kutoka shilingi 1500 hadi 2000 kwa kimoja
" Tatizo ni uhaba
wa nafaka na protini iliyotokana na kukumbwa na mabadiliko ya tabia ya nchi
hasa ukame kiasi cha wafanyabiashara wa chakula kutupandishia bei kulingana na
wanavyopata lakini kupunja baadhi ya protini na virutubisho kwenye kuchanganya
vyakula hii inawafanya kuku kuishi bandani
kwa zaidi ya siku tano hadi 10 za ziada kutoka Ile 30 hadi 35 anayopaswa
kuuzwa"
"Mbaya zaidi
unakuta chakula hakuna ubora hivyo unapompa kuku unaweza kumsababishia kudumaa
au kupata magonjwa mbali mbali yanayopelekea vifo kwa kukosa virutubisho muhim
au magonjwa yatokanayo na sumu kuvu endapo malighafi za kutengeneza chakula
hayakuhifadhiwa vyema"
Alisema kuwa
kutokana na hayo wafugaji wamekuwa watumwa wa kutumia madawa mbali mbali na
kemikali za hatari kukuzia kuku bila kujali afya za walaji ili tu
kunusuru biashara zao
Nae meneja wa kampuni
ya bidhaa za kuku kutoka trouw Nutrition, Joseph Joachim Alisema kuwa
wako jijini Arusha kuwapa mafunzo zaidi wafugaji jinsi ya kutumia bidhaa za
asili kutoka vya mimea na matunda kukuzia kuku bila madawa yenye kemikali
zinazoathiri zaidi walaji wao ambao ni binadamu.
Alisema kuwa
changamoto kubwa katika ufugaji ni magonjwa mbali mbali yanayowapata kuku
inayotoka na asili ya kifaranga alipototolewa, hali ya hewa, maji na chakula
hasa visivyo na virutubisho vya kutosha au vilivyopatwa na ugonjwa sumu kuvu.
"Haya yote
yanawalazimu wafugaji kutumia madawa mengi hata yaliyo hatari kwa walaji kwa
kusababisha magojwa ya kansa lakini watatumia kuokoa kuku wao, kutokana na hilo
tumekuja kuwapa suluhu la bidhaa kadhaa
za kuwasaidia kutibu kifaranga akiwa mdogo, maji yao ya kunywa lakini pia
virutubisho mbali mbali vya chakula Ili kuokoa kuku kudumaa na hizi hazina
madhara wala kemikali"
Alisema kuwa sekta ya
ufugaji wa kuku unakua zaidi nchini kutoka kuku milioni 44 kwa miaka mitano
iliyopita hadi milioni 92 pamoja na changamoto nyingi zinazokatisha tamaa wanazokabiliana
nazo hasa chakula kuwa ghali na vifaranga huku bei ya kuku ikibakia ndogo hivyo
kuiomba serikali kutoa bei elekezi ya vyakula vya kuku na kuku wenyewe sokoni.