LATRA yazipiga marufuku bajaji Arusha

 

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) mkoa wa Arusha,  Amani Mwakalebela,akizungumza kwenye kikao hicho cha mkuu wa wilaya ya Arusha mjini Said Mtanda  (nne kulia)


Bertha Mollel , Arusha


Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) imesitisha  usajili mpya wa bajaji kufanya kazi za usafirishaji ndani ya jiji la Arusha ili kufanya uhakiki wa zilizopo.


Hayo yamesemwa na Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) mkoa wa Arusha,  Amani Mwakalebela,  alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa madereva bajaji wa jiji la Arusha ulioitishwa na mkuu wa wilaya ya Arusha mjini Kwa ajili ya kuunda umoja wao na kufanya uchaguzi wa viongozi.

Mwakalebela alisema kuwa wameamua kisitisha utoaji wa leseni mpya kutokana na wingi wa bajaji zilizopo tofauti na hali halisi ya zilizosajiliwa.

"Bajaji zilizosajiliwa hazizidi 1000 lakini zinazofanya kazi ziko zaidi ya 3000, na mbaya zaidi wanafanya kazi zilizo nje ya usajili wao, hali inayoibua migogoro kila kukicha baina ya bajaji na daladala" alisema Mwakalebela

Alisema kuwa bajaji zinatakiwa kukaa kwenye kituo na kukodiwa kama bodaboda au kujaza abiria katika kituo kimoja lakini badala yake wamekuwa wakiokota abiria barabarani na wengine kufikia hatua ya kupiga debe kazi inayotakiwa kufanywa na daladala.

"Hali hiyo imeibua migogoro sana baina ya watoa huduma hao wawili hadi kufikia kusababisha migomo ya hapa na pale sasa nawaomba muwe na nidhamu ya kazi kwani hatutasita kuendelea kutoa adhabu mbali mbali kwenu" alisema na kuongeza...

"Kwa sasa bajaji zimetosha kwenye jiji la Arusha, na kama upo hapa na hujasajiliwa anza kutafuta wilaya nyingine ya kwenda, na anaetaka kununua bajaji aambiwe kabisa hakuna usajili wa kufanya kazi hapa hadi tufanye uhakiki wa zilizopo kama hazijakidhi mahitaji tutaongeza usajili wa chache na kama zimetosha ndio basi tena" 

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Arusha mjini, Said Mtanda alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kuwasaidia maderava bajaji kuwa na umoja wao unaotambulika na serikali lakini pia kufanya uchaguzi wa viongozi wao ili kuweza kupatiwa fursa mbali mbali zinazotolewa na serikali pamoja na Taasisi mbali mbali.

Alisema kuwa madereva bajaji katika jiji la Arusha wamekuwa wakisababisha migogoro mingi baina yao na madereva daladala kutokana na kuingiliana katika majukumu huku wanaoonywa wanakaidi maagizo mbali mbali.

"Mmekuwa kama familia ya kambale,  kila mmoja ana sharubu, Sasa kuanzia sasa nataka ni 'deal' na nyie jino kwa jino na nitaomba ushirikiano wenu wale wasamaria wema tusaidiane kuwakamata wanaotumia kigezo Cha bajaji kufanya uhalifu" alisema na kuongeza...

"Wakaidi wote nataka majina yao, hadi wale wanaojifanya wanaendesha vyombo vya wakubwa au vigogo wajue siogopi mtu yoyote tutawakamata wao na vyombo vyao kisha tutawapeleka kule jeshini (JKT oljoro) wakafundishwe uzalendo kidogo ndani ya mwenzi mmoja tutawatoa tena" alisema Mtanda.

Mtanda alitumia mkutano huo, kujadili na kupitisha katiba ya umoja wa bajaji ndani ya jijia Arusha (Uwabaja) sambamba na kuunda kamati ya kuratibu mchakato mzima wa uchaguzi ndani ya siku 14.


Kwa upande wake mkuu wa kikosi cha usalama barabarani, SP Solomon Mwangamilo alisema kuwa moja ya kundi kubwa linalowaumiza kichwa jeshi la polisi ni madereva bajaji kutokana na ukaidi wao wa kufuata sheria za usalama barabarani huku baadhi yao wakiongoza kufanya uhalifu kupitia vyombo vyao.

"Baadhi ya wahalifu wamekuwa wakipitia hapo hapo kufanya uhalifu na sisi kama polisi tunashindwa hata tumuone nani, yaani mmezidi dharau sana.., kuanzia sasa tutanyooshana hasa kwenye adhabu za kawaida na zile mnazozuia maafisa wasitekeleze wajibu wao kwenu maana tumechoka kiwavumilia"alisema Kamanda Mwangamilo.

Kaimu mkurugenzi wa jiji la Arusha Hargeney Chitukuro aliwataka madereva hao kuhakikisha wanafuata sheria ya kulipa ushuru wa maegesho katika vituo vyao ili kuepuka migogoro na migongano na uongozi wa halmashauri.

Nae mwenyekiti wa mpito wa 'Uwabaja', Joseph Mwita alisema kuwa changamoto kubwa ni usajili na vituo vya maegesho, huku wakiiomba serikali kuwaongezea mda wa kujisajili Latra ili kujiendesha kihalali

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!