Manyara.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara imezuia kuzikwa kwa miili ya watu watatu wanaodaiwa kufariki kwa kunywa pombe yenye sumu hadi uchunguzi wa kitaalamu ukamilike.
Watu hao Madai Amsi 'Samweli' (42), Hao Bado (59) na Nada Yaho 'Paulina' (43) wakazi wa Kijiji cha Bashnet wilayani Babati mkoa wa Manyara walifariki dunia January 31,2025 kwa nyakati tofauti huku wakidaiwa vifo vyao kusababishwa na kunywa pombe Kali yenye sumu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani amesema kuwa bado vifo hivyo vina utata wa chanzo halisi cha tukio hivyo wamezuia kwanza isizikwe ili kukamilisha taratibu za kiuchunguzi wa kitaalamu kwa ajili ya hatua za kisheria.
“Watu hao wanadaiwa wamefariki kwa kunywa pombe yenye sumu lakini hatuwezi kuwa na uhakika labda walikunywa kuzidisha kiwango chao au kunywa pombe kali bila kula au vyovyote ndio maana tumezuia katika hospitali ya wilaya ya Babati kwa taratibu za kuichunguzi wa kitaalamu” amesema.
Awali wakizungumza nyumbani kwao , mke wa marehemu Samweli, (Veronika Daniel) amesema kuwa siku ya tukio mume alitoka kwenda kunywa pombe kabla ya kurudi usiku na kwenda kulala.
“Asubuhi mimi niliamka kwenda shambani na niliporudi mchana ndio nikashangaa kumkuta mume wangu amelala akidai anaumwa sana tumbo na kichwa, nilimpa maji na nikimtaka apumzike lakini baadae kidogo alianza kutapika mfululizo kabla ya kelegea.
“Tulipoona hivyo tulimchukua na kumpeleka hospitali ya Bashnet na kutundikiwa dripu za maji lakini kwa bahati mbaya haikuchukua mda mrefu alifariki dunia”.
Mwenyekiti wa maafa katika kijiji cha Bashnet, Samweli Manda amesema kuwa wamepata taarifa za vifo hivyo ambapo ameiomba serikali kuchukua hatua za haraka kuchunguza tukio hilo
Amesema kuwa siku ya tukio alipata taarifa za kuzidiwa kwa Paulina (Nada) kwa madai kuwa masaa machache yalipopita alikunywa pombe, wakati wanafanya taratibu za kuwahisha hospitali alifariki.
“Watu walimpeleka mochwari alfajiri hiyo na kufanya taratibu zote za kuhifadhi mwili na wakarudi nyumbani lakini wakakutana taarifa zingine kuwa kuna mzee (Hao) amezidiwa aliyekuwa anakunywa na marehemu jana”.
“Nae alipelekwa kituo cha afya Bashnet kwa machela maana hali ilikuwa mbaya na kutundikiwa dripu lakini saa saba mchana alifariki”.
Amesema kuwa wakati wanawaza vifo hivyo ndio walipata taarifa za Madai (Samweli)nae amefariki akipatiwa matibabu.
“Hapo ndio vichwa vikaanza kuuma watu wakiwaza ni nini ndio wakapata habari kuwa wote walikuwa wanakunywa pombe pamoja, hivyo tukaanza kutilia shaka pombe hiyo"amesema .
Alitumia nafasi hiyo kutoa ombi kwa serikali "Tunaomba serikali ichunguze kwa kina inawezekana pombe hiyo ilikuwa na sumu iliyosababisha vifo vya wenzetu mana kila siku wanakunywa iweje leo wafe tena kwa wakati mmoja na dalilia moja?” amesema.
Nae mjumbe wa serikali ya Kijiji cha Bashnet, Agripina Tango amesema kuwa unywaji wa pombe katika eneo hilo imekuwa kero kubwa hasa wafanyabiashara kusambaza kileo hicho kwenye majumba ya watu asubuhi na kusababisha baadhi ya watu kuwa waraibu.
“Serikali tunaomba iingilie kati swala hili maana si jambo la kwanza watu kuzidiwa na kilevi na hii ni kutokana na watu wengi wamekuwa waraibu wa pombe zinazotembezwa mitaani asubuhi kila kukicha na kusababisha nguvu kazi ya Taifa kupotea kutokana na wengi wanaotumia pombe hizo kuwa ni vijana na wazee wanaotegemewa na familia
Mwisho.