Arusha.
Wananchi wa Kanda ya kaskazini wametaka maendeleo ya sayansi na Teknolojia iegemee kwenye uvumbuzi zitakazitumika kukuza na kuimarisha uchumi nchini utakakuwa wenye ushindani kwenye soko la dunia.
Wananchi hao wameyasema hayo kwenye kongamano la pili la Kikanda kuhusu maandalizi ya dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 iliyofanyika Leo katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano ya AICC iliyofanyika Jijini Arusha.
Mshiriki Elias Mollel amesema kuwa kipindi hiki ambacho dunia iko kwenye ulimwengu wa kidigitali, wanatamani dira ya 2050 ilete fursa mbali mbali za teknolojia itakayoongeza uchumi mifukoni mwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Isiwe tunajisifu tuko kwenye ulimwengu wa kidigitali ambao hautusaidii kutatua changamoto yetu kubwa ambayo ni uchumi, bali dira ituelekeze sasa kunufaika na hatimae kupiga hatua kutoka nchi inayoendelea na kuwa nchi iliyoendelea” amesema Mollel kutoka Tanga.
Nae Rehema Mollel alisema kuwa katika dira ya 2050 wanatamani kuona Mageuzi ya kweli ya kiuchumi hivyo iko haja ya kujenga uchumi madhubuti , jumuishi, endelevu, shindani na stahimilivu.
“Nikisema hivyo namaanisha kuwa kujengwe fursa kwenye Nyanja mbali za utalii, ufugaji, kilimo,Uvuvi na sekta ya madini pamoja na wajasiriamali pia wafanyabiashara”
Hivyo kuanzia sasa serikali ione jinsi gani ya kuzikuza sekta hizo zote ziwe na tija lakini pia ziwekewe mazingira wezeshi ya kuzifanikisha.
Akifungua kongamano hilo, Waziri wa nchi ofisi ya Rais mipango Na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amewataka wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru na usawa dhidi ya Tanzania waitakayo kwa miaka 25 ijayo.
Alisema Lengo la dira hiyo ni kuinua ustawi wa watanzania kama nyenzo mama ya kuimarisha na kudumisha uhuru na furaha kwa kila mtanzania na nchi kwa ujumla ambayo watazingatia pia uzoefu wa nchi zilizoendelea ili kufikia ustawi wa juu wa mafanikio.
“Katika hilo hatuna budi kuweka mkazo kwenye mageuzi makubwa ya Kiuchumi, Elimu, Afya , Kilimo na miundo mbinu ili kufanikisha hayo” amesema Profesa Mkumbo.
Kwa upande wake Mjumbe wa tume ya Mipango, Neema Mduma amesema kuwa katika maoni yaliyotolewa tangu kuanza kwa zoezi hilo kwa njia mbali mbali ikiwemo ujumbe mfupi, tovuti na kongamano la kwanza la Kikanda Mkoani Mwanza, wameshaona uelekeo wa nini watanzania wanataka katika dira ya mwaka 2050.
“Wengi wamesema mageuzi ya kiuchumi, matumizi ya Teknolojia, lakini pia wanataka dira iegemee kwenye maendeleo ya watu na jamii ikiwemo uboreshwaji wa huduma kwenye sekta mbalimbali” amesema Neema.
Mbali na hilo amesema kuwa maoni mengi pia wananchi yanataka utawala bora, haki, Ulinzi, na Usalama huku wakitaka pia kuona viongozi wanawajibika wanapokutwa na makosa lakini pia wametaka matumizi bora na sahihi ya rasilimali za Taifa hasa zitumike kwenye kuinua maendeleo".