Waziri Bashungwa ataka vituo vya afya vyote kunakuwa na dirisha la wazee

NA OR-TAMISEMI


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Innocent  Bashungwa ametoa maelekezo kwa wakurugenzi wote nchini kuhakikisha vituo vyote vya afya kunakuwa na dirisha la wazee na muda wote kuwe kuna muuguzi ambaye anahakikisha wazee wanapata matibabu bila shida yoyote.

 

Pia  Bashungwa ametoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Morogoro kusimamia majengo ya Kituo cha Afya cha Nhembo ambayo yapo kwenye asilimia 70 hadi 75 ifikapo Agosti, mwaka huu mwishoni majengo yote yawe yameshakamilika.

Katika ziara yake wilayani Klosa mkoani Morogoro, Mheshimiwa Bashungwa pia amemuagiza RMO kufanya utaratibu wa usajili wa kituo hicho angalau kuanza huduma kwa ngazi ya zahanati huku kituo kikiwa kinaendelea kukamilika.

Amesema ifikapo Septemba Mosi,mwaka huu huduma ndogo ndogo zianze kutolewa kwa wananchi waanze kuzipata huku kituo kikiendelea kukamilika.


Aidha, amesema kwa majengo mapya ambayo fedha imekuja na bado haijatumika viongozi wamepewa mpaka Desemba kuhakikisha fedha hiyo na majengo hayo mapya yawe yameshakamilika.

 

Mheshimiwa Bashungwa amesema, Mkuu wa mkoa akifika na kukuta maelekezo hayo bado hayajafanyiwa kazi, basi achukuwe hatua stahiki.
Amesema, fedha zinapokuja kwenye maeneo ya kata kwa malengo ya kujenga vituo vya afya viongozi ni jukumu lao kuhakikisha wanasimamia ili kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!