Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) wakishirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wamefanikiwa kusaini Mkataba wa makubaliano wa utengenezaji wa Dira 100 za Maji za Malipo ya kabla ya matumizi (pre-paid) utakaosaidia kuondoa changamoto mbali mbali za maji nchini.
Mkataba huo uliosainiwa mjini Dodoma jana, umeshuhudiwa na Waziri wa Maji Jumaa Aweso na Naibu Waziri wa Elimu, sayansi na Teknolojia, Omary Juma Kipanga.
Akizungumza wakati wa kusaini Mkataba huo, Aweso alisema ATC imekuwa Msaada mkubwa kwa Taasisi za serikali hapa nchini hasa katika bunifu zao mbali mbali.
“Leo hii tungewaza kuagiza Dira za maji kutoka nje ya Nchi lakini tukasema ni vema kukatumia wataalamu wetu wa ndani wenye ujuzi katika kusaidi taifa letu na leo ATC imekuwa moja ya msaada wetu kwa utaalamu huo” alisema,
Aweso aliitaka ATC kutengeneza Dira Bora zitakazouzwa kwa bei nafuu zitakazovutia Hadi soko la nje na kukuza Ajira lakini zaidi kutatua changamoto ya huduma za vijijini ambayo ndio hitajio la serikali kwa sasa.
Kwa upande wake, Kipanga alisema kuwa wizara yake inajivunia kuwa na vyuo vya ufundi kutokana na kunufaika na bunifu zake ikiwemo chuo Cha ATC ambacho kimekuwa na majibu ya changamoto mbali mbali ambayo zingeigharimu Serikali kutumia wataalam wa nje kuzitatua.
"Niliwahi kutembelea pale ATC Arusha na kujionea kwa jinsi gani teknolojia hii ya malipo ya kabla inavyofanya kazi hakika najivunia nao sana kwani mbali na bunifu hiyo bado kuna mambo mengi na mazuri yanakuja kupitia chuo hichi” alisema Naibu Waziri Kipanga.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Clement Kivegalo amesema mkataba huo, ATC katika hatua za awali itatakiwa kubuni na kufunga Dira za maji 100 zitakazombazwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya majaribio kwa kipindi cha miezi sita.
“kuna faida za kutumia wataalamu wetu wa ndani katika miradi mbali mbali hivyo ATC kubuni dira hizi serikali inanufaina na tutendelea kuwapa sapoti kwani Itaboresha uhusiano wa taasisi zetu za umma, na zaidi itaboresha huduma zetu kwa ukaribu zaidi"
Nae mhandisi wa chuo cha Ufundi Arusha alisema ATC kinatarajia kuanza rasmi utengenezaji na ufungaji wa dira 100 za maji za malipo ya kabla ya matumizi na zitasambazwa katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya majaribio(Pilot Study) kwa kipindi cha miezi.
Aidha dira hizi zimebuniwa na wataalam kutoka chuo cha Ufundi Arusha.