![]() |
Prof. Gabriel Shirima Mlau wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela akiongoza maandamano wakati wa sherehe za mahafali Agosti 29, 2024 Kampasi ya Tengeru Arusha. |
Arusha.
Wataalamu wa maswala ya Sayansi, Teknolojia na mazingira wameanza utafiti wa uhakika wa upatikanaji wa Mahitaji muhimu katika kukabiliana na ongezeko kubwa la watu nchini.
Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, Tanzania imekuwa na ongezeko la watu kwa asilimia 37, kutoka watu milioni 44.92 waliokuwepo mwaka 2012 hadi kufikia watu milioni 61.74.
Hata hivyo, hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa limekadiria kuwa Tanzania inaweza kuwa na watu mara mbili ya ilivyo sasa ambayo ni zaidi ya watu milioni 120 ifikapo mwaka 2050.
Kutokana na hayo, Wataalamu wa Maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Mazingira wameanza kuchukua tahadhari ya ongezeko hilo hasa katika upatikanaji wa Mahitaji muhimu kama Chakula, na maji, lakini pia usalama wa mazingira na mawasiliano.
Akizungumza katika mahafali ya 10 ya Wahitimu 92 wa shahada ya Uzamili na Uzamivu katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), mmoja wa watafiti hao, Denis Amos Mwalongo amesema kuwa sababu kubwa ya kufanya utafiti huo ni ili serikali ipate namna bora ya kukabiliano na ongezeko la watu na iwe fursa badala ya tatizo.
“Sisi watafiti hatufai kukaa na kusubiri tatizo litokee maana itakuwa hatuna maana kwenye nchi zetu, tunaona viashiria vya tatizo na kuanza utafiti wa kutatua, ndio maana tumeanza utafiti mapema wa ongezeko la watu maana tatizo halitakuwa idadi bali jinsi ya kupata mahitaji muhimu”
“Moja ya hitaji ni chakula, tunafaa kujiuliza ardhi haiongezeki lakini tunaongezeka hivyo ni jinsi gani tutajilisha ukizingatia kila siku majanga ya uharibifu wa mazingira unapelekea ukame na mafuriko”Amesema na kuogeza;
“Lakini pia tunawekeza nguvu kuona namna gani mazingira yatabaki salama kutokana na ongezeko la watu hasa katika utunzaji wa bionuwai zilizopo kwa ustawi wa sisi binadamu na viumbe wengine” amesema.
Utafiti huo pia utalenga upatikanaji endelevu wa maji safi na salama ambapo Mwalongo amesema kuwa inaweza kuhatarisha maisha ya watu baadae kutokana na mahitaji kuongezeka lakini vyanzo vya maji vizidi kupungua kutokana na ukuaji wa miji.
“Hitaji ligine kubwa ni mawasiliano ya uhakika hasa kwa nchi yetu ya Tanzania ambayo inakwenda kuwa na idadi kubwa ya vijana, ambao watahitaji ajira, lakini tatizo hilo linaweza kutatuliwa kwa uhakika wa mawasiliano hasa ya watakapotumia mitandao kwa manufaa ya kibiashara na kusaka fursa za uwekezaji” amesema Mwalongo.
![]() |
Akizungumza katika mahafali hayo, Makamu Mkuu wa Chuo cha NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula alisema asilimia 85 ya wanafunzi waliohitimu kutoka nchi mbalimbali wamepata udhamini wa masomo yao kutokana na tafiti mbalimbali za kutatua changamoto za kijamii wanazozifanya.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka kuwa sehemu ya mageuzi ya kijamii, na kiuchumi yanayoendelea nchini na duniani kote hasa katika matumizi ya teknolojia za akili mnemba( AI), Roboti na mashine ya kuhisi.
“Zaidi mkatumie maarifa na ujuzi mliopata kuchangamkia fursa zinazoendana na teknolojia za kidigiti hasa katika kuendeleza sayansi, uhandisi na ubunifu unaolenga kuleta mageuzi katika sekta ya kiuchumi hasa uzalishaji na huduma”
Mwisho……..