Tanzania yavuna kampuni tatu za uwekezaji nchini China kwenye sekta ya mawasiliano


China

Kampuni tatu kutoka nchini China zimeonyesha nia ya kutaka kuwekeza kwenye Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hapa nchini.
 

Kampuni hizo ni pamoja na China Academy of Space Corporation (CASC) inayojishughulisha na masuala ya uundaji na urushaji wa satelaiti, na nyingine ni China Electronics Corporation iliyoonesha nia ya kuwekeza katika Ujenzi wa Kiwanda cha kutengeneza vifaa vya TEHAMA pamoja na Kampuni ya Transsion Group.

Tanzania imevuna kampuni hizo mara baada ya mazungumzo kati ya Rais wa Tanzania,  Dk. Samia Suluhu Hassan, dhidi ya Wawekezaji na Viongozi wa Kampuni mbalimbali zilizopo nchini China ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi nchini humo. 


Katika Mkutano huo, Rais Samia amekuwa na mazungumzo na Viongozi wa Kampuni za China Academy of Space Corporation (CASC), China Electronics Corporation, Transsion Group, Weihua Group, China Railway Construction Corporation (CRCC) pamoja na Acme Consultant Engineers PTE Limited na CND zote za China.

Akizungumza Leo Septemba 6,2024 jijini Beijing nchini China, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla, amesema Wizara hiyo ipo tayari kushirikiana na wawekezaji hao na wengine watakaojitojeza kwenye sekta yake.

 Abdulla amesema Wizara imekwishaandaa programu itakayojulikana kwa jina la “From the Peak of Mount Kilimanjaro to Space” itakayohusu uundaji na urushaji wa satelaiti itakayoanza mwaka huu.

"Tunawakaribisha wenzetu waje tufanye kazi na tunawaahidi kuwapokea na kuwapa ushirikiano wote utakaohitajika kwa ajili ya kufanikisha uwekezaji wao hapa nchini"amesema Abdullah.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!