Arusha.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya kaskazini Godbless Lema amefanikiwa kuzindua rasmi Operesheni Kucha Mkoa wa Arusha kwa kishindo inayolenga kuhamasisha wananchi kukataa dhuluma za uchaguzi ujao.
Katika Uzinduzi huo, Lema amesema kuwa awamu hii hatakimbia tena nchi na kwenda kuwa mkimbizi kwenye nchi ya watu kisa uchaguzi.
Amesema kwa sasa amejipanga na yuko tiyari kudhurika lakini sio kuonewa kama ilivyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Lema aliyewahi kuwa M'bunge wa Arusha Mjini alikimbilia nchini Kanada mwaka 2020 mara baada ya uchaguzi Mkuu wa madiwani, Wabunge na Rais kwa kile alichodai kuhofia maisha yake kabla ya kurejea mwaka jana 2023 mwezi Februari.
"Safari hii sitakubaki kuonewa, hata kama nikipigwa risasi lakini sitakubali kizembe wala kuonewa tutakula sahani moja nao kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa haki na Uhuru" amesema Lema.
Mbali na hilo Lema amewataka wananchi wa Arusha kuacha unafki linapokuja swala la wanapambania haki zao kwani wanaporudi nyuma na kuwaacha viongozi wao wenyewe wanawakatisha tamaa.
"Hakuna watu wanakatisha tamaa nchi hii kama nyie wananchi, hapa tunaongea mikakati ya uchaguzi lakini baada ya mda mnarudi nyuma wote na kutuacha wenyewe tunapopata shida"
"Mnasababisha hadi baadhi ya viongozi wenye Moyo mdogo wanahama chama kwa sababu yenu, ndio maana siwalaumu hata wakina David Silinde na Mchungaji Peter Msigwa waliokimbia kwa sababu ya hatma ya maisha yao" amesema Lema .
Amesema kuwa katika watu waliokamatwa mara nyingi na kuwekwa Polisi au kufungwa magereza na yeye yumo lakini ni kwa sababu ya kupigania haki za wananchi ambao wamerudi nyuma kisiasa.
"Mimi hata ikitokea lolote sasa hivi Sina deni na umma, na hata nikifa sasa hivi Sina deni na Mungu maana kati ya watu waliogombana na viongozi wakubwa wa nchi, kuwekwa Polisi na magereza ni Mimi lakini hakuna mtu aliyeandamana hata kupinga ukatili huu tunaofanyiwa na akina Tundu Lissu" amesema Lema.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kukataa michezo yoyote michafu inayofanyika kwa ajili ya kuufanya uchaguzi usiwe na Uhuru na haki.
"Kuanzia sasa hivi chukueni fomu, na kama Kuna mtu unamjua ana sifa nenda kamshawishi achukue fomu na nawahakikishia mkifanya hivyo tutapata viongozi wenye vitu waliotokana na Wananchi na nawaambia tutashinda sana endapo mtakuja kushiriki uchaguzi bila hofu wala kurubuniwa"
Awali Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amewataka wananchi kuhakikisha wanashiriki hatua zote za uchaguzi na wasilagaiwe na mtu yoyote kwani mwaka huu hawatasusia uchaguzi.
"Miaka mitano tuliyowaachia imewatosha waliopita, na Wananchi wamenyimwa haki yao vya kutosha, hakikisheni mwaka huu hamkai nyuma kushiriki mchakato mzima wa uchaguzi na mkagombee Ili tupate watu wenye uzalendo" amesema Golugwa.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure alisema kuwa lengo la operesheni kucha ni kukataa michezo yote michafu inayofanywa kipindi cha uchaguzi kwa ajili ya kuufanya isiwe wa huru na haki.
"Safari hii msikubali watu wanaokuja kwenye nyumba zenu na kuwataka vitambulisho vyenu au kuwahonga chochote kununua haki zenu, huo sio wakati wa kanga na pombe bali ni kazi tu kuhakikisha tunarudisha Jimbo letu kwa kuanza na wenyeviti wa mitaa" amesema Mungure.