Bertha Mollel - Arusha
Wakulima wa kahawa mkoani Arusha wameiomba Serikali kutoa ufumbuzi wa dawa za magonjwa na wadudu wanaoshambulia zao hilo.
Wakizungumza katika maonyesho ya nane nane, walipotembelewa katika banda la halmashauri ya jiji la Arusha, wakulima hao walisema kuwa zao la kahawa kwa Sasa linaweza kuwa na tija kubwa endapo Serikali utaweza kupata ufumbuzi wa madawa yanayoweza kudhibiti visumbufu vya zao hilo.
Rehema Jackson alisema Bei ya kahawa iliyopo sokoni imerudisha wakulima wake, changamoto kubwa ni magonjwa na wadudu wanaoshambulia miti na matunda hali inayoshusha kiwango cha mavuno.
"Bei ya kahawa kutoka 1000 kwa kilo hadi kufika 5000 imeleta mvuto kwa Wakulima wa Arusha kurudi kutumikia zao hili tatizo kubwa ni wadudu wanaoshambulia miti, lakini magonjwa kama mnyako fusari, CBD na kitu vimekuwa kikwazo"
"Tunaomba Serikali itafute njia m'badala wa kudhibiti visumbufu hivi kwani dawa tulizoletewa madukani hazifanyi kazi kwa ufanisi hasa za kuuwa wadudu kwenye miti"
Nae Robert Mollel alisema kuwa kahawa imekuwa na soko kubwa hasa nje ya nje hivyo wanaomba Serikali iwawezeshe Wakulima wenye Nia ya kulima kahawa kwa mikopo ya pembejeo ikiwemo miche na viuatilifu.
"Mkulima anaweza kuvuna zao hili kwa miaka miwili mfululizo hivyo hawezi kukosa kurejesha fedha alizowezeshwa ukizingatia ukubwa wa Bei na soko la kahawa nchini hivyo tunaomba Serikali litusaidie Wakulima"
Akijibu ombi Hilo, mkuu wa wilaya ya Arumeru eng. Richard Ruyango alisema kuwa bado Serikali inafanya uwekezaji mkubwa kwenye zao hilo hivyo kuwaondoa hofu Wakulima juu ya changamoto ya viuatilifu.
"Serikali chini ya uongozi wa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan bado Ina mipango mikubwa na zao hili na naamini watafiti wako kazini kwa ajili ya kazi hiyo na ufumbuzi utapatikana mapema Sana"
Ruyango pia aliwataka Wakulima hao kuhamasisha watanzania wengi kutumia kahawa kutokana na faida zake nyingi lengo ikiwa ni kuongeza watumiaji wengi wa ndani kwa soko endelevu lakini kuzuia mtikisiko wa bei endapo soko la kimataifa likiyumba.