Na mwandishi wetu.
MGANGA
Mkuu wa Serikali, Dkt.Aifello Sichalwe amesema, Serikali kupitia Wizara
ya Afya na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(OR-TAMISEMI) imelenga kupunguza vifo vya Wajawazito na watoto kupitia
mikataba itakayobeba viashiria vya wajawazito na lishe inayotarajiwa
kusainiwa na Wakuu wa Mikoa.
Dkt.
Sichalwe ameyasema hayo katika kikao cha Wadau wa Sekta ya Afya kwenye
eneo la mama na mtoto pamoja na Lishe kilichofanyika Mkoani Singida.
"Tumekubaliana
kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais aliyoyatoa ya kuja na mkataba mmoja
ambao utakuwa umebeba viashiria vya utendaji vya akina mama wajawazito
pamoja na masuala ya Lishe ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa
kupambana dhidi ya vifo vya Wajawazito na watoto wachanga,"amesema
Dkt.Sichalwe.
Aliendelea
kusema kuwa, pamoja na hayo Serikali kwa kushirikiana na wadau
imekubaliana kuanza kutekeleza matumizi ya kanzi data, yatakayotoa fursa
ya kujua viashiria vya hatari vya mjamzito endapo anavyo kutokana na
maswali atayoulizwa na Mtaalamu wa afya.
Sambamba
na hilo Dkt. Sichalwe amesema, kwa upande mwingine Serikali kwa
kushirikiana na wadau wamekubaliana utekelezaji wa azimio la vikao vya
kujadili vifo vya mama na mtoto vilivyoanzishwa na Wizara ya Afya
kikanda.
Aidha,
Dkt. Sichalwe ameeleza kuwa, kwa pamoja kama Wadau wa Sekta ya Afya
wamekubaliana kutekeleza mfumo wa kusimamia magari ya kubebea Wajawazito
(M-MAM) unaorahisisha mfumo wa rufaa nchini kama sehemu nyingine ya
mkakati wa kupambana dhidi ya changamoto ya vifo vya Wajawazito na
watoto.
Mbali
na hayo, Dkt. Sichalwe amewashukuru Wadau waliojitokeza katika kikao
hicho cha Kimkakati na kuweka wazi kuwa, maazimio yote ya kikao hicho
yatawasilishwa kwenye uongozi wa Wizara ya Afya na TAMISEMI kwaajili ya
utekelezaji na Wadau wote walioshiriki kikao hicho na wasio shiriki
watakuwa katika utekelezaji.
Hata
hivyo, ameweka wazi kuwa, wamekubaliana kuleta mipango yao, namna
walivyotekeleza na changamoto wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa
mipango hiyo na wanaishauri nini Serikali ili kwa pamoja kuona namna
gani wanaweza kushirikiana kuzitatua kwa lengo la kuongeza kasi ya
kupunguza vifo vya mama na mtoto katika jamii.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi
ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema, katika kikao hicho
wamepitia viashiria mbalimbali vinavyolenga masuala ya mama na mtoto
ambavyo vitasaidia kuongeza uwajibikaji kwa viongozi mbalimbali ngazi ya
Mkoa na kupima matokeo ya uwajibikaji huo kwa kupungua kwa vifo vya
Wajawazito na watoto.
Pia,
Dkt. Ntuli amesema kuwa, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa
miundombinu ambapo vituo vya afya 650 ambavyo vinatoa huduma za upasuaji
vimejengwa, huku hospitali mpya za Halmashauri 130 zikijengwa, hivyo
uwekezaji huo ni lazima uende sambamba na huduma bora zitazosaidia
kupungua kwa vifo vya Wajawazito na watoto.
"Serikali
imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu, katika kipindi cha miaka
mitano vituo vya afya 650 vinavyotoa huduma za upasuaji, sambamba na
hilo hospitali mpya za Halmashauri 130, sasa uwekezaji huo lazima uende
sambamba na huduma,"amesema Dkt.Ntuli.