NEMC yatangaza bomoa bomoa Arusha waliovamia vyanzo vya maji




Arusha. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), imetangaza kufanya zoezi la bomoa bomoa makazi na shughuli zote za kibinadamu zilizovamia vyanzo vya maji.

Akizungumza mkoani Arusha, Mkurugenzi mkuu wa NEMC, Dkt. Samwel Gwamaka alisema wanatarajia kutekeleza zoezi hilo baada ya kumaliza majadiliano na watu wa misitu na ardhi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji.

"Sheria yetu ya mazingira hairuhusu shughuli zozote za kibinadam hasa ujenzi ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji, lakini uvamizi mkubwa unaendelea,"alisema na kuongeza..

" Sasa niwaambie wahusika tutafanya bomoa bomoa na kufyeka mazao yote yaliyoko ndani ya hifadhi na kamata kamata isiyo na Kikomo ya mifugo na watu pia"

Gwamaka aliwatupia lawama kubwa watu wa mipango miji kuwa adui mkubwa wa mazingira kutokana na kupanga miji kwenye maeneo yanayotegemewa kuleta uhai katika vyanzo vya maji"

"Watu wa mipango miji ndio maadui wakubwa wa mazingira, na hili nalisema bila kupepesa macho kwa sababu eti ni wenzetu wa Serikalini,..wao wanapanga miji Hadi kwenye milima wakati wanajua fika hizo ndio vyanzo vya uhai wa maji,"

Gwamaka alisema kuwa NEMC kwa Sasa wako katika maboresho ya Sheria mpya ya mazingira inayotarajia kuanza kutumika mwishoni mwa mwaka huu ambao utaweza kuwapa meno zaidi ya kutatua changamoto za mazingira ikiwemo utoaji wa vibali kwa wawekezaji.

"Tunafanya maboresho ya Sheria ya mwaka 2004, ambayo itapunguza majukumu ya waziri kwa kutuwezesha kutoa Hadi vibali kwa wawekezaji hasa vile visivyo hatarishi kwa mazingira"





 Akizungumza wakati wa zoezi la uwekaji wa alama 'bikon' za mita 60 pembezoni mwa mito mkoani Arusha, Mkurugenzi wa bodi ya maji katika bonde la Pangani Segule Segule alisema zoezi hilo linaenda sambamba na tathimini ya shughuli za binadamu zilizovamia vyanzo hivyo. 

Alisema kuwa wao Kama wasimamizi wa maji yanayotoka bonde la pangani wanahakikisha matumizi ya binadamu dhidi ya maji hayo hayaathiri binadamu Wala vyanzo vyenyewe.

"Tunaweka hizi Bikon kuwakumbusha watumiaji wa maji wasiingie katika maeneo ya hifadhi, kwa ajili ya matumizi endelevu ya maji, na baada ya kukamilisha zoezi hili katika mito yote Arusha tutatoa majibu ya nyumba na shughuli ngapi zimevamia na hatua za kisheria tunazochukua dhidi yao"

Segule aliwataka wananchi wanaofanya shughuli zozote ndani ya hifadhi ya vyanzo vya maji kuacha Mara moja kabla Sheria haijachukua mkondo wake dhidi yao.

Nae mwenyekiti wa watumia maji ya mto Themi, Samwel Laizer alisema kuwa shughuli za binadamu zinazofanyika katika maeneo ya vyanzo vya maji hasa mito inawaweka katika hatari kubwa ya magonjwa ya mlipuko na ukame wa maji wananchi wanaoishi ukanda wa chini.

"Tunaomba Serikali itusaidie kuzuia hizi shughuli hizi maana Kuna watu wanaosha magari na kutiririsha maji machafu ndani ya Mito, wengine wanafulia ndani  na zaidi wako wanaolima mboga na kuchunga kwenye mito" 

Alisema shughuli zote hizo zinawaweka katika hatari ya kukosa maji lakini hata yakija ni machafu Hali inayowaweka katika hatari ya kuugua magonjwa ya mlipuko hasa kuhara na kipindu pindu kwa watumiaji.
Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!