DCEA Kanda ya kaskazini imeteketeza Kilogramu 204.8165 za dawa za kulevya





Arusha

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini  kwa niaba ya Kamishna Jenerali, imeteketeza  Kilogramu 204.8165 za dawa za kulevya katika Dampo la Muriet lililopo katika Jijini la Arusha jana January 29,2025

 

Katika Kilogramu 204.8165 zilizoteketezwa, mirungi ilikuwa ni Kilogramu 172.8165 na bangi kavu ilikuwa Kilogramu 32.0 yote ikihusisha jumla ya  watuhumiwa 33 waliokamatwa kwa makosa ya kupatikana na dawa hizo.


 Kati ya waliokamatwa,   watuhumiwa Wanaume ni 25 na Wanawake ni Nane.


Watuhumiwa hao kwa mujibu wa DCEA, walikamatwa katika operesheni zilizofanyika kuanzia Januari 2024 hadi Januari 27, 2025 katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara. 


Taratibu za uteketezaji wa  vielelezo hivyo umefanyika kwa kuzingatia sheria na miongozo husika ambapo Mahakama ya Wilaya ya Arusha iliridhia vielelezo hivyo viteketezwe kwa kuwa vikikaa muda mrefu vinaweza kupoteza uhalisia na hata kupelekea kuharibika. 


Aidha, Watuhumiwa Saba katika miongoni mwa Watuhumiwa 33 waliokamatwa na dawa hizo tayari kesi zao zilishatolewa hukumu za vifungo Mwaka 2024 na kesi  nyingine zinaendelea katika Mahakama za ngazi ya Mikoa na Wilaya katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara. 


Taasisi za Serikali zilizopo mkoani Arusha zikihusisha Afisa Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkoa wa Arusha, Afisa kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Kaskazini, Hakimu Mkazi Mwandamizi kutoka Mahakama ya Arusha na Afisa Mazingira kutoka Halmashauri ya Jiji la Arusha wote hao kwa mujibu wa takwa la kisheria walishiriki katika uteketezaji wa Kilogramu 204.8165 za dawa za kulevya katika Dampo la Muriet jijini Arusha.


Mwisho

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post
Alert: Content is protected !!